Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA Freeman Mbowe akkihutubia wakazi wa Jiji la Mbeya na vitongoji vyake hivi karibuni |
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa uzinduzi wa zoezi la upigaji kura unaofanyika mjini Makambako mkoani Njombe ni kiini macho cha kuwadanganya wananchi kuwa tunaelekea kwenye uchaguzi wa haki na sawa ifikapo Oktoba 31 mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA Freeman Mbowe alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Baraza la uongozi la chama hicho kanda ya nyanda za juu kusini kwenye ukumbi wa Hotel ya Diamond iliyopo Sae Jijini Mbeya jana.
Mbowe alisema kuwa mchakato mzima wa uandikishaji na zoezi la uandikishaji wapiga kura umekuwa na usiri mkubwa kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Chama tawala ilhali viongozi wakuu wa vyama vingine vya siasa hawajui kinachoendelea.
''Mimi ni kiongozi wa CHADEMA sijiu chochote kinachoendelea juu uandikishaji wapiga kura, tukumbuke zimebaki siku chache kuelekea uchaguzi Mkuu, kalenda ya uchaguzi mkuu inafahamika kikatiba, lakini kumekuwa na ukiritimba mkubwa unaofanywa na Tume ya Uchaguzi''alisema.
Alifafanua kuwa yeye amealikwa dakika za mwisho kuhudhuria uzinduzi wa Kitaifa wa uandikishaji wapiga kura mjini Makambako na kuwa utaratibu mzima unaofanywa hauna tija kwa walengwa kwani zoezi hilo litafanyika kwenye kata 9 za mji huo badala ya jimbo zima au mkoa kwa ujumla.
''Huu ni uharibifu wa fedha za wananchi, uzinduzi unafanywa kwa kata 9 pekee za mjini Makambako,badala ya kufanyika jimbo zima, kuna kitu kinafichwa hapa haiwezekani zoezi hili lifanyike kwa kata chache huku mahitaji ni wananchi wote wajiandikishe katika daftari la kudumu la wapiga kura nchini,''alifafanua.
Alisema kuwa seriikali ilimuomba mtaalamu mwelekezi wa masuala ya uandikishaji wapiga kura kutoka nchini Marekani Darrel Geusez ambaye alitakiwa kusaidia uandaaji wa mfumo wa kielekroniki ''Biometrict Voters Registration'' (BVR).
Mbowe alisema Mtaalamu huyo baada ya kufanya utafiti wake alitoa majibu ya kuwa haitowezekana kwa daftari hilo kuboreshwa na kukamilika kwa kipindi kifupi kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba na kwamba maandalizi ya mfumo huo yanatakiwa kuchukua mwaka mzima ili uandikishaji uende kwa taratibu zinazostahili.
''Kutokana na hili ni vigumu kuingia katika uchaguzi bila kuwepo kwa uchakachuzi,nimealikwa kuhudhuria uzinduzi huu, niambieni ndugu zangu niende au nisiende,''alihoji Mbowe mbele ya wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Kanda wa chama hicho.
Baada ya kuhoji umati wa wajumbe wa mkutano huo kutoka mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma walipaaza sauti hewani kwa kusema, ''Usiendeee!!!, Mbowe aliwahoji mara tatu wajumbe hao na kujibiwa hivyo hivyo ndipo alipotoa kauli kuwa yeye hawezi kushiriki uzinduzi huo.
''Siwezi kushiriki uzinduzi huo, nikishiriki nitakuwa nimebarikli uchakachuaji huu, nitakuwa nimeshiriki kuhujumu Watanzania, siwezi kwenda,''alisisitiza Mbowe huku akishangiliwa na wajumbe hao.
Awali Mbowe akizungumza na vikosi vya ulinzi vya chama hicho Red Brigedi alisema kuwa vikundi hivyo vya chama tofauti na vile vya chama cha Mapinduzi vinalenga kuwafundisha uzalendo,ujasiriamali,maadili na kusimamia uchaguzi ifikapo Oktoba 31.
''Nataka watambue kuwa CHADEMA ni chama cha siasa wala si jeshi, sisi tunafanya mambo yetu hadharani lakini wenzetu wanafanya kwa kificho, wanafanya mafunzo ya kijeshi na kufanya vurugu kwenye uchaguzi mkuu, nendeni mkaoneshe nidhamu ya chama bila kujali itikadi,''alisema.